Jumatatu 23 Novemba 2026 - 12:00
Wanaharakati wa Shahidi Ahmad Zakzaky (r.a) washiriki mkusanyiko wa usiku wa wananchi wa Iran mjini Qum

Hawza/ Wanaharakati wa Shahidi Ahmad Zakzaky (r.a) (JASAZ) katika Jamhuri ya Kiislamu ya Iran, wameshiriki katika mkusanyiko wa usiku wa wananchi wa Iran uliofanyika katika Uwanja wa Sheikh Mufid, mjini Qum, ambapo wameonesha mshikamano wao na wananchi wa Iran pamoja na misimamo yao ya kuunga mkono Wilaya.

Kwa mujibu wa Shirika la Habari la Hawza, Wanaharakati wa Shahidi Ahmad Zakzaky (r.a), ambalo ni miongoni mwa taasisi zinazohusishwa na Harakati ya Kiislamu ya Nigeria inayoongozwa na Hujjatul-Islam wal-Muslimin Sheikh Ibrahim Zakzaky, walishiriki katika mkusanyiko wa usiku wa wananchi wa Iran uliofanyika katika Uwanja wa Sheikh Mufid, mjini Qum, Jumatano usiku, Novemba 19, 2026 (27 Aban 1405).

Mkusanyiko huo ni sehemu ya mfululizo wa shughuli za usiku zinazofanywa na wananchi wa Iran. Shughuli hizo huwashirikisha watu kutoka makundi mbalimbali ya jamii katika maeneo tofauti ya nchi, kwa lengo la kufanya upya ahadi ya utiifu kwa Kiongozi wa Mapinduzi ya Kiislamu, pamoja na kusisitiza kuendelea kushikamana na Wilaya. Mkusanyiko huo ulikuwa ni wa usiku wa 263 katika mfululizo wa mikusanyiko hiyo.

Ushiriki wa Wanaharakati wa Shahidi Ahmad Zakzaky, katika shughuli hiyo ulikuwa sehemu ya programu za wiki ya kuadhimisha kumbukumbu ya kuzaliwa Shahidi Ahmad Zakzaky, iliyofanyika mjini Qum.

Wakati wa mkusanyiko huo, kikundi cha uimbaji kiliwasilisha nyimbo za hamasa zenye maudhui mbalimbali, zikieleza misingi ya kiitikadi na malengo ya mapambano ya harakati hiyo. Nyimbo hizo ziliwavutia washiriki wa mkusanyiko huo.

Aidha, tamko la taasisi hiyo lilisomwa. Katika tamko hilo, taasisi hiyo ilitangaza mshikamano na kuwaunga mkono wananchi wa Iran, huku ikipongeza juhudi na msimamo thabiti wa wananchi wa Iran pamoja na harakati nyingine za Muqawama katika kutetea haki, kupambana na dhuluma, kuwaunga mkono waliodhulumiwa na kuunga mkono Wilaya.

Mwisho wa hafla hiyo, Sheikh Nur Muhammad, mmoja wa viongozi wa Wanaharakati wa Shahidi Ahmad Zakzaky (r.a) katika Jamhuri ya Kiislamu ya Iran, alitoa hotuba fupi kuhusu mitazamo ya taasisi hiyo juu ya umuhimu wa kuunga mkono Wilaya na mshikamano baina ya mataifa na harakati zinazopigania haki.

Shahidi Ahmad Zakzaky, alikuwa mmoja wa watoto watatu wa Sheikh Ibrahim Zakzaky waliouawa na serikali ya Nigeria wakati wa maandamano ya Siku ya Quds mwaka 2014. Kwa baraka za damu ya shahidi huyo, mamilioni ya vijana wamepata mwamko na kuamua kuiendeleza njia yake.

Lebo

Maoni yako

You are replying to: .
captcha